Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kitaifa imetakiwa kukabiliana na maafisa wafisadi kama njia moja ya kuokoa uchumi wa Kenya ambao umetajwa kutokuwa imara.

Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Elementaita, mjini Gilgil, wakati wa kukagua mradi wa maji, Seneta mteule wa Nakuru Martha Wangari, alisema kwamba ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mkaguzi wa hesabu za serikali ameweka bayana kwamba shilingi bilioni 400 zilipotea mwaka huu kutokana na ufisadi.

Wangari alisema ni vigumu kwa miradi mikuu ya serikali kama vile ile ya reli ya kisasa ya SGR kuafikiwa endapo hali hii ya ufisadi itazidi kushuhudiwa hapa nchini.

“Ni muhimu kwa tume ya kukabiliana na ufisadi ya EACC kuchukua hatua mwafaka kwa kufanya uchunguzi ambao utapelekea maafisa walio na mazoea hayo kufikishwa mahakamani,”alisema Wangari.

Seneta huyo alisema idara ya mahakama inafaa kupiga jeki juhudi za tume hiyo za kukabiliana na ufisadi kwa kuhakikisha kwamba haki inatendeka na hatua kuchukuliwa dhidi ya wanaobainika kuwa wafisadi.

Alisema kwamba hatua ya kwanza ya kuhakikisha hilo ni kwa jaji mkuu Dkt Willy Mutunga kuhakikisha maafisa wafisadi wa idara ya mahakama wanaondolewa.

Isitoshe, Wangari alisisitiza kuwa ni jambo la kuvunja moyo kuona kwamba serikali inakosa kuafikia matakwa na mahitaji mbalimbali kama vile ya kuwapa walimu nyongeza ya mishahara ilhali baadhi ya maafisa wa serikali wanaiba mali ya umma.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa kupanda kwa gharama ya maisha kutamtatiza mwananchi wa kawaida.

Wangari alisema kuwa kupanda kwa gharama hiyo kunatokana na ufisadi ambao umesababisha kuongezwa kwa ushuru wa vifaa kama vile pikipiki ambazo zimepelekea vijana wengi kujiajiri.