Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar ameshikilia msimamo wake wa kupigania demokrasia ya nchi ili kuhakikisha kuwa maswala muhimu nchini yanatekelezwa kwa usawa.
Akizungumza katika eneo bunge la Changamwe mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Omar alisema kuwa njia pekee ya kuhakikisha kuwa taifa hili linazingatia usawa wa utekelezaji wa maswala muhimu kwa mwananchi sharti demokrasia kupiganiwa kikamilifu.
Omar alisema kuwa ukosefu wa elimu kwa baadhi ya jamii nchini kumepelekea kuwepo na ugumu wa kufanikisha ajenda muhimu mashinani.
Seneta huyo aliahidi kuanzisha hamasa kwa jamii ili kufahamu demokrasia vyema.
Wakati huo huo aliwataka wakaazi wa eneo bunge la Changamwe na Kaunti ya Mombasa kwa jumla kuhakikisha kuwa wanajitenga na viongozi walaghai wasio na azma yoyote ya kuwafanyia maendeleo, na kuwachagua viongozi waadilifu wakati wa uchaguzi mkuu.
"Nitahakikisha kuwa demokrasia inalindwa na kupiganiwa kikamilifu ili maswala muhimu katika Kaunti ya Mombasa kutekelezwa,” alisema Omar.
Seneta huyo wa Kaunti ya Mombasa ametangaza kuwania ugavana katika uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2017.