Seneta Hassan Omar amemkosoa Spika wa Kaunti ya Mombasa Thadius Rajwayi kufuatia matamshi yake kuhusu maseneta.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada ya spika huyo kuwashutumu maseneta ambao wana azma ya kuwania viti vya ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

"Bunge la Seneti ni idara yenye umuhimu sana nchini kwa kutoa mwelekeo wa ugatuzi na kuunda sheria zinazohusiana na kaunti na utendakazi wake,” alisema Rajwayi.

Seneta Omar kwa upande wake alitofautiana na kauli hiyo ya spika wa kaunti ya Mombasa, kwa kusema kuwa maseneta wana haki ya kuwania viti hivyo vya ugavana.

"Kila Mkenya ana haki ya kuwania wadhifa wowote ule katika kaunti na hata serikali kuu. Nawahimiza hasa spika wenywewe waongoze shughuli za ugatuzi katika kaunti zao na wala sio kutumika kama chombo cha magavana katika shughuli za kaunti,” alisema Seneta Omar.

Aliongeza, “Namhimiza Spika Thadius kufanya kazi kulingana na sheria iliyowekwa na sio kutumika kama mlinzii wa gavana katika shughuli za kaunti.”

Spika huyo alikuwa akizungumza siku ya Jumatatu katika kongamano la maseneta na wawakilishi wadi kutoka kaunti zote 47, mjini Mombasa.