Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amekashifu vikali hatua ya mataifa ya kigeni kuweka ilani ya kutozuru baadhi ya sehemu nchini kutokana na ukosefu wa usalama.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Omar amesema kuwa balozi wa Marekani humu nchini Robert Godec, anafaa kufunga virago vyake na kuondoka nchini, iwapo anahisi kuwa kuna utovu wa usalama.

Akizungumza katika hafla ya usalama iliyopangwa na kampuni ya Safaricom ikishirikiana na muungano wa wakaazi wa maeneo ya Mombasa al maarufu Kara siku ya Ijumaa katika hoteli moja jijini Nairobi, Omar alisema kuwa visa vya ugaidi havifai kuwa vinapelekea mataifa ya Ughaibuni kuwekea Kenya vikwazo.

Seneta huyo alisema kuwa taifa lolote linaweza kupatikana na mashambulizi.

“Kama viongozi na Wakenya wote kwa jumla, hatuwezi kubali kuchafuliwa jina la taifa ilhali ugaidi ni jambo ambalo limekue janga la ulimwengu wote,” alisema Omar.

Aidha, Seneta Omar alikashifu mataifa hayo kwa kuiharibia Kenya sifa, kwa kusema ni kinaya ikizingatiwa kuwa kuna mauaji ya ndani kwa ndani na hata visa zaidi vya ugaidi kwa mataifa hayo ikilinganishwa na Kenya.