Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amewakosoa Gavana Hassan Joho na Rais Uhuru Kenyatta kwa kurushiana cheche za maneno badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Omar amewataka wawili hao kuasi tofauti zao za kisiasa na kuhudumia watu wa Mombasa kwa kuanzisha miradi ya maendeleo.
“Si vizuri kurushiana maneno, twataka maendeleo yafanyiwe watu wa Mombasa,” alisema Omar.
Seneta huyo alisema kuwa vijana wengi Mombasa hawana ajira na sharti Joho na Uhuru washirikiane katika kuboresha maisha ya vijana ambao wengi wanajihusisha na uhalifu.
“Vijana hawana ajira na wengi wanajihusisha na ujambazi na ugaidi ili kukidhi mahitaji yao,” alisema Omar.
Kauli hii inajiri baada ya Gavana Joho kumkashifu hadharani Raisi Kenyatta kuhusu miradi ya Jubilee jijini Mombasa.
Wakati huo huo, amekashifu namna wamiliki wa bunduki wanavyotumia silaha hizo kiholela, akisema kuwa lazima sheria za kumiliki bunduki zitiliwe mkazo ili kuepuka vitisho kwa wananchi.