Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip. Picha-NMG.
Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip amesema kuwa atayataja majina ya watu ambao wamenyakua zaidi ya ekari 350,000 za ardhi ambazo hati miliki za ardhi hizo zilitwaliwa na tume ya ardhi nchini mwaka wa 2015.
Hati miliki hizo zilitwaliwa baada ya kugunduliwa kuwa zilipatikana kwa njia ya mkato na kupeanwa kwa serikali ya kaunti ya Lamu kwa uangalizi wa ardhi hizo.
Hata hivyo, Loitiptip anasema kuwa wengi hawafahamu kuwa ardhi hizo zilinyakuliwa tena na watu Fulani kwa njia za kisiri.
Loitiptip alisema pia atayataja majina ya watu wengine ambao wamekuwa wakiendesha biashara haramu ya madawa ya kulevya na hivyo kulemaza juhudi za serikali za kupigana na madawa ya kulevya eneo hilo.
Akizungumza mjini Lamu siku ya Jumatatu, Loitiptip alisema kuwa majina hayo ni ya wanasiasa, wakuu wa usalama, matajiri na wakuu wa nyumba kumi ambao amewataja kama wanaolemaza juhudi zake za vita dhidi ya madawa ya kulevya na unyakuzi wa ardhi.
“Niko na majina ya zaidi ya watu 20 ambao wamenyakua maelfu ya ekari ya mashamba na wengine zaidi ya kumi ambao wanaendeleza biashara ya madawa ya kulevya,’’ alisema Loitiptip.
Afisa mkuu katika idara ya mashamba kaunti ya Lamu ambaye alikataa jina lake lisitajwe alisema kuwa ekari 350,000 ya shamba ilinyakuliwa.