Seneta wa kaunti ya Nyamira Mong'are Okong'o amewataka vinara wa muungano wa Cord kumteua mmoja wao ili kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wanahabari kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumatano, Mong'are alisema kuwa yafaa vinara wa muungano wa kisiasa wa Cord kumteua mmoja wao atakaye wania urais mwakana.

"Cord ni muungano dhabiti sana na wenye wafuasi kutoka kila pembe ya taifa hili, na kwa sababu tumesalia na miezi michache ili tuelekee kwenye uchaguzi mkuu ujao ningependa kuwasihi vinara wa Cord kumtawaza mmoja wao ili awe ndiye atakayewania urais mwakani kwa maana hii hali ya kila mtu kujitangaza kuwa ndiye atakayewania urais inawakanganya wakenya," alisema Mong'are. 

Mong'are aidha alimtaka gavana wa kaunti ya Nyamira kutafuta mbinu ya kusuluhisha mzozo wa umiliki wa mji wa Keroka kwa haraka ili kuwaepusha wakazi wa eneo hilo na visa vya kuibuka vita mara kwa mara. 

"Nadhani wakati umefika kwa gavana Nyagarama kuchukua hatua kuhakikisha kuwa mzozo wa umiliki wa mji wa Keroka baina ya serikali yake na ile ya Kisii unasuluhishwa kwa haraka ili kuwaepusha wakazi wa eneo hilo na vitavita vya mara kwa mara," aliongezea Mong'are.