Kwa mara nyingine tena seneta wa Kaunti ya Nyamira Okongo Mongare amejitokeza kuwashtumu vikali wawakilishi wadi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira kwa kutotekeleza majukumu yao ya uangalizi jinsi inavyostahili.
Kwenye ujumbe alioutoa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, Mong'are alisema kuwa wawakilishi wadi wa bunge la kaunti hiyo wameshindwa kutekeleza majukumu yao inavyostahili huku wakiwatetea maafisa wakuu wa serikali ya kaunti hiyo dhidi ya ufisadi.
"Wawakilishi wadi wamefeli pakubwa katika utekelezaji wa majukumu yao kikatiba na sasa wamegeuka kuwatetea mawaziri ambao wanahusishwa na sakata za ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka," alisema Mongare.
Hata hivyo, seneta Mong'are aliwapa changamoto wawakilishi wadi kuidhinisha ripoti ya kamati ya uhasibu wa pesa za umma ili mawaziri wanaohusishwa na ufisadi wawajibikie vitendo vyao.
"Sio bunge lote ambalo kwa hakika limetufeli kama kaunti kwa maana kamati ya uhasibu na uwekezaji wa pesa za umma inatekeleza majukumu yao inavyostahili ila ninawapa changamoto wawakilishi hao kuhakikisha kuwa ripoti ya kamati hiyo inaidhinishwa ikiwa kwa kweli wamejitolea kupambana na ufisadi," aliongezea Mong'are.
Ikumbukwe kuwa kamati ya uhasibu na uwekezaji wa pesa za umma PIAC kwenye bunge la kaunti hiyo iliandaa ripoti iliyopendekeza mawaziri wafisadi kuchukuliwa hatua kali ila ripoti hiyo ikakataliwa bungeni mwezi michache iliyopita.