Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are amejitokeza kumshtumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kutenga eneo la Gusii kimaendeleo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa chumba cha maankuli kwa wanafunzi wa shule ya upili ya Egentubi siku ya ijumaa, Mong'are alisema kuwa Rais Kenyatta amekuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo kila anapozuru maeneo ya kati, mashariki na Bonde la Ufa mwa nchini huku akitenga eneo la Gusii. 

"Kwa kweli Rais Uhuru ni kama amelitenga eneo la Gusii kimaendeleo kwa sababu kila anapozuru maeneo ya kati, mashariki na bonde la ufa lazima miradi mikubwa ya maendeleo izinduliwe katika maeneo hayo, na ni aibu kwamba anapokuja Gusii, kazi yake ni kuwaambia watu wa jamii ya Gusii waungane na Jubilee," alisema Mong'are. 

Mong'are aidha aliongeza kwa kuitaka serikali kuchukua hatua ya kuhakikisha eneo la Gusii linafaidi kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo, la sivyo eneo la Gusii liendelee kuipinga serikali. 

"Anachostahili kujua rais Uhuru ni kuwa yeye ni rais wa jamii 42 za wakenya na wala sio jamii mbili tu, na haya maneno yao ya kututaka kujiunga na serikali ni ndoto iwapo miradi mhimu ya kimaendeleo itakayowasaidia watu wetu haitozinduliwa Gusii," aliongezea Mong'are.