Seneta wa kaunti ya Nyamira amemtaka gavana wa kaunti hiyo kuhakikisha wafanyakazi wa vibarua wanalipwa pesa zao.
Senata huyo pia amewataka wafanyikazi hao kupewa kipaumbele katika kazi ambazo zimetangazwa na kaunti hiyo.
Akiongea na waandishi wa habari katika mji wa Nyamira siku ya Jumatatu, Seneta Okong’o Omang’are alishangazwa na swala hilo la kaunti hiyo kutowalipa wafanyakazi hao wa vibarua.
Alisema kuwa kuna pesa zilizotengwa kushughulikia malipo ya wahudumu wote wa kaunti ambao hufanya kazi katika vitengo mbali mbali katika kaunti hiyo.
Mong’are alimtaka gavana wa kaunti ya hiyo, John Nyagarama kuwajibikia maswala yanayomlenga.
Alimtaka gavana kushughulikia swala hilo liloripotiwa katika vyombo vya habari kuhusiana na vibarua ambao wanahudumu katika hospitali ya Nyamira level five ambao wamekuwa wakilalamikia kutolipwa hela zao kwa muda sasa.
“Ningependa gavana Nyagarama kulishughulikia swala hilo la wafanyakazi kutolipwa haraka iwezekavyo ili kila mtu atendewe haki kulingana na katiba na sheria za kusimamia wafanyakazi,” alisema Seneta Mong’are.
Seneta huyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa gavana wa kaunti hiyo yake kwa siku za hivi karibuni.