Maseneta wametishia kupinga miswada miwili muhimu iliyopendekezwa na bunge la kitaifa kufuatia mzozo kuhusu kutafsiriwa kwa sheria hizo.
Bunge la seneti na lile la kitaifa yanatofautiana pakubwa kuhusu tafsiri ya mswada unaopendekeza maspika wa mabunge hayo yote kupeana ruhusa kabla ya sheria yoyote ama mswada wowote unaopendekezwa kukubaliwa.
Miswada iliyopendekezwa hivi karibuni ni pamoja na mswada kuhusu kilimo, uvuvi miongoni mwa miswada mingine ambayo tayari imekubaliwa na kupitishwa na wabunge na kwa sasa, miswada hiyo ipo mbele ya bunge la seneti.
Maseneta wamemtuhumu spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi kwa usemi kuwa hajatilia maanani mswada unaowahitaji maspika wa mabunge yote mawili kuchunguza miswada na kisha kuuamua ni bunge lipi linafaa kufanya uamuzi kwenye miswada hiyo. Aidha, maseneta wamekataa kuangazia miswada hiyo kwa usemi kuwa miswada hiyo haikuwasilishwa kwa njia inayofaa kwani maspika wote wawili hawakukutana jinsi inavyohitajika katika kifungu cha 110 (3) cha katiba.
Maseneta hao wamesisitiza kuwa wataanzisha mchakato wa miswada hiyo kwa misingi kuwa bunge la seneti litavunja miswada hiyo.