Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i amesema serikali haitatumia pesa zake kujenga mabweni za shule ambazo huchomwa na wasiojulikana.
Hii ni baada ya shule tatu za eneo moja katika kaunti ya Kisii kuchomwa wakati mmoja jambo ambalo limeleta mzozo mkubwa.
Kulingana na Matiang’i mabweni ya shule za upili za wavulana ya Nyamagwa, wasichana wa Nyamagwa na ya mseto Nyamagwa yalichomwa wakati mmoja mapema wiki hii na kusema serikali haitatumia pesa kujenga mabweni hayo ambayo huchomwa.
“Mimi kama waziri wa elimu nawahakikishia wakaazi wa Kisii haswa wale wako karibu na shule hizi za upili za Nyamagwa kuwa serikali hakuna vile itatumia pesa kujenga mabweni hayo liwe liwalo maana mabweni hayo yanachomwa na watu,” alisema Matiang’i.
Matiangi pia alisema ikiwa wanakijiji wanahitaji walimu wakuu kutolewa karibu na maeneo yao ya makaazi ili kusimamia shule hizo wasahahu kamwe kwani hilo halitafanyika.
“Kuna hii tabia ya wakaazi kutaka mwalimu mkuu awe anasimamia shule iliyoko karibu na kwake na hilo halitafanyika katika shule hizo za Kisii maana hatutaki mambo ya kuleta ukabila,” aliongezea Matiang’i.