Serikali na tume huru ya mipaka na uchaguzi -IEBC- ziitalaumiwa iwapo patatokea machafuko ya aina yoyote kabla ,wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Kulingana ana aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA jimbo la Nakuru Abdul Noor, serikali na IEBC watabeba lawama kwa kukataa kuitikia mwito wa wakenya wa kuwataka makamishina wa tume hiyo kung'atuka afisini.
Akizungumza Jumanne mjini Nakuru, Noor aliitaka serikali na IEBC kuiepushia nchi balaa kwa kusikiza malalamishi ya upinzani.
Aidha, alimtaka rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kuwashawishi makamishna hao wa IEBC kuondoka kwa hiari.
“Iwapo nchi itakumbwa na machafuko mwaka 2017 basi watakao laumiwa ni rais na serikali yake pamoja na IEBC kwa sababu itasemekana walikataa kutilia maanani wito wa wakenya,” alisema Noor.
“Mimi ningetoa wito kwa rais kulichukulia swala hili kwa uzito na kuwashawishi maafisa wa IEBC kujiondoa afisini kwa hiari ili kuliepushia taifa balaa,” aliongeza.