Wakaazi wa eneo la Likia huko Mau Narok walifanya maandamano ya amani Jumatano, kulalamikia serikali ya Jubilee kwa kuwatelekeza wakati ambapo wakimbizi wa ndani kwa ndani wanafidiwa.
Wakaazi hao wengi wao wakiwa ni wakimbizi wa mwaka wa 1992, 1997 na 2007/8, pia wanajumuisha watu waliofurushwa msituni mwakani wa 1988.
Wakiongozwa na mzee Pius Mburu, wakaazi hao wameisuta serikali kwa kufidia baadhi ya wakimbizi na kuwaacha wao wakiteseka bila makao maalum.
Aidha mzee huyo amesema wengi wao wamepewa makao na majirani katika eneo la Likia, na wanakaa maisha ya umaskini kutokana na serikali kutowafidia.
“Serikali imekuwa ikitupuuza kwa miaka mingi, na sasa tumeonelea kuandamana ili kufahamisha ulimwengu kwamba kuna IDPs na watu waliotolewa msituni mwakani wa 1988 hapa Likia ambao hawajafidiwa,” alisema Pius Mburu.
Mwandishi huyu amezungumza na MCA wa wadi hiyo Irungu Gitonga ambaye amekiri kwamba hakuna mtu hata mmoja wa Likia ambaye ni IDP alipokea shilingi elfu mia nne, zilizotolewa maajuzi na serikali kufidia wakimbizi.
“Ukiona maisha ambayo hawa wakimbizi na waliokuwa walowezi wa msitu wa serikali wanaishi utawahurumia. Wae wa 2007/8 wanakaa katika hema zilizochanika, na wale wa 1992, 1997 kurudi hadi 1988, bado hawana makao kwa sababu nyumba zao zilichomwa.”
“Likia ndio huadhirika zaidi na vita vya kikabila vinapozuka sehemu hii, na kwa hivyo kama sehemu zingine tunahitaji kuwaonyesha jinsi ya kuishi kwa umoja, na uwiano. Uwiano huo unaanza kwa wao kupokea fidia kutoka kwa serikali,” alisisitiza.