Waakazi katika Kata ya Naishi kwenye Kaunti ndogo ya Njoro wamelalamikia ukosefu wa maadili miongoni mwa Machifu wa eneo hilo huku wakiitaka serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Wakaazi hao wamesema kuwa licha ya maafisa wa serikali kutakiwa kutekeleza majukumu yao kwa njia ya uwazi, Machifu na Naibu wao wamekuwa wakidai malipo kwa kila huduma wanazotoa kwa wananchi, jambo ambalo limechangia wananchi kulalamikia utendakazi wao.
Wamesema machifu hao fisadi wamekuwa wakiwafungia macho wapishi wa pombe haramu huku wanaoendeleza biashara hiyo wakitoa rushwa ili hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao.
Aidha wenyeji hao wamesema kwamba kwa sasa hawana imani na Chifu na Naibu wake huku wakiongeza kuwa serikali iliwapa kazi maafisa hao licha na kwamba wao si wenyeji wa maeneo wanayowakilisha.
Naibu kamshina wa Njoro Mohamed Hassan ambaye alipokea barua ya malalamishi kutoka kwa wakaazi hao ametoa amri kwa Machifu husika kufika mbele ya kamati ya usalama ili kujibu hoja zilizotolewa na umma dhidi yao.
Wakaazi hao wametishia kufanya maandamano iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa dhidi ya Machifu hao ambao wamedai wamezembea kazini.