Naibu Rais William Ruto amesema serikali ya kitaifa itaimarisha zaidi ufugaji na kilimo ili wakulima na wafugaji wanufaike zaidi kama njia moja ya kupunguza umaskini.
Ruto ametangaza kupunguzwa kwa bei ya mbegu za uzalishaji wa Ng’ombe almaarufu 'Artificial Insemination' kutoka shillingi 2,000 hadi 500 ili kuimarisha ufugaji katika taifa la Kenya.
Akizungumza siku ya Jumapili katika uwanja wa Nyamache eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii, Ruto alitangaza bei hiyo mpya ya Sh500 huku akisema serikali ya kitaifa itanunulia kaunti ya Kisii mashine 10 za kuhifadhi maziwa almaarufu ‘Milk Coolers’ ambazo zitagharimu shillingi millioni 110 ili kutumika kuzuia maziwa kutochacha.
“Mbegu ya ng’ombe ilikuwa inapeanwa kwa shillingi 2, 000 na bei hiyo imepunguzwa kwanzia leo hadi Sh500 ili ufugaji uimarike zaidi,” aliongeza Ruto .
Ruto aliomba wakaazi kukumbatia ufugaji na kilimo ili kupunguza hali ya umaskini katika jamii zao huku akisema serikali ya kitaifa itaendelea kusaidia wakulima hao ili wafaulu kupitia ufugaji na kilimo.
Aidha, aliomba serikali za kaunti kushirikiana na ile ya kitaifa kuhakikisha hali ya umaskini imepunguzwa katika jamii mbalimbali.