Katibu mkuu katika Wizara ya vijana na jinsia Zeinab Hussein, amesema serikali inapanga kujenga vituo vya kuwasaidia waathiriwa wa dhulma za kijinsia katika kaunti 20 humu nchini.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Hussein alisema kuwa vituo hivyo vitatumika kutoa msaada kwa waathiriwa katika maeneo yanayongoza katika dhulma hizo, ikiwemo Kaunti ya Mombasa.

‘’Waathiriwa wengi wanakosa namna ya kupata msaada baada ya kupitia dhulma. Ni kutokana na hilo ambapo serikali sasa inataka kuweka mpangilio utakaohakikisha kuwa waathiriwa hawa wanasaidiwa kuyarejelea maisha yao ya kawaidia,’’ alisema Bi Hussein.

Aidha, alisema serikali itazindua mpango utakao wahusisha viongozi wa kidini, viongozi wa kijamii na wahudumu wa matatu katika hatua inayonuia kupunguza ongezeko la dhulma za kijinsia hasa kwa wanawake.

‘’Vita dhidi ya dhulma za kijinsia vinahitaji ushirikiano. Lazima tufanye kazi na kila idara ili kuhakikisha kuwa tunaziba mianya yote ambayo wanaoeneza dhulma hizi wanatumia,’’ aliongeza.

Hussein vilevile alisema serikali inashirikiana na idara za mahakama kuhakikisha kuwa washusika wa dhulma za kijinsia wanachukuliwa hatua kali za ksiheria.