Serikali kuu kupitia kwa Wizara ya Maji inanuia kusambaza maji safi katika shule zote humu nchini kama njia mojawapo ya kufikisha huduma hiyo kwa wananchi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa kudumu katika Wizara ya Maji Fred Sugor amesema kuwa bado kuna uhaba wa maji safi nchini ikizingatiwa kuwa ni asilimia 58 tu ya watu ambao hupata maji safi.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Mombasa wakati wa kongamano la wadau wa mazingira, katibu huyo alisema kuwa wizara hiyo pia imeweka mikakati ya kusafisha maji ya bahari ambayo kwa kawaida huwa na chumvi nyingi, ili yaweze kutumika nyumbani.

"Tuko katika harakati za kutafuta wadhamini watakaotuwezesha kubuni njia ya kusafisha maji ya chumvi kutoka baharini ili yaweze kutumiwa nyumbani kwa matumizi ya kawaida,” alisema Sugor.

Sugor alisema kuwa changamoto ya uhaba wa maji katika eneo la Pwani itatatuliwa iwapo mradi huo utazinduliwa.

Haya yanajiri huku eneo la Pwani likiendelea kushuhidia uhaba wa maji safi.

Kampuni ya maji ya Coast Water Board imelazimika kukatiza huduma zake kufuatia serikali za kaunti kukosa kugharamia deni la mamilioni ya pesa kwa kampuni hiyo.