Wanawake kutoka Kaunti ndogo ya Ganze na Mombasa wameitaka serikali kuu na ile ya kaunti ya Kilifi na Mombasa iwapelekee vifaa vya kupimia maradhi ya saratani mashinani ili waweze kuyatambua maradhi ya ugonjwa huo mapema.
Wakiongozwa na Mshirikishi wa sauti ya wanawake Judith Uchi, wanawake hao walisema kuwa wengi wao wamepoteza maisha kutokana na maradhi hayo ambayo yanaweza kutibika iwapo yatatambulika mapema.
Judith aliwashinikiza wanawake kuhakikisha kuwa wanajitokeza kwa wingi na kupima maradhi yao ambayo yamekuwa sugu kwa jamii ili kufahamu hali zao za kiafya na jinsi ya kukabilia na mara kama hayo.
“Wakati umefika sasa akina mama kuhakikisha kuwa hamuogopi tena kuhusu kupima maradhi ya Saratani ili kujua hali zenu za kiafya na jinsi ya kujikinga, japo tuko katika mastari wa mbele kuishinikiza serikali kuleta vifaa ya kupima saratani mashinani,” alisema Judith siku ya Ijumaa mjini Mombasa kwenye mkutano wa maendeleo ya wanawake.
Aidha, waliitaka wizara ya Afya nchini na zile za kaunti ya Kilifi na Mombasa ziongeze idadi ya dawa katika zahanati.