Serikali ya kitaifa imelaumiwa kwa kuingilia sekta zilioko chini ya uongozi wa serikali za kaunti.
Hii ni baada ya kamishena wa kaunti ya Kisii Chege Mwangi kuagiza kufungwa kwa viwanda vidogo vidogo 21 vya kutengeneza sukari nguru katika eneo bunge la Mugirango kusini kaunti ya Kisii .
Akizungumza siku ya Jumatano mjini Kisii, naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amelaumu serikali ya kitaifa kwa kuingilia sekta za serikali za ugatuzi, huku akisema sekta ya kilimo iko chini ya uongozi wa serikali za ugatuzi na hakuna vile viwanda hivyo vitafungwa kamwe.
Maangi alisema serikali hiyo ilichukua hatua hiyo kupitia kamishena Mwangi bila kufahamisha serikali ya kaunti ya Kisii na kusema ni vibaya hatua kuchukuliwa bila serikali hiyo kujulishwa.
“Hatujafurahishwa jinsi serikali ya kitaifa inafunga viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sukari nguru maana wengi wanategemea sukari nguru kusomesha wanao,” alisema Maangi.
Ata hivyo, Maangi aliwahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kuwa watulivu serikali ya ugatuzi inapopanga kuandaa kikao na serikali ya kitaifa kuondoa agizo hilo ambalo linaonekana kuwanyanyasa wakazi hao.