Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko ameishinikiza serikali kuu kutenga fedha zaidi kwa serikali za kaunti ili kuboresha sekta ya afya.
Akiongea katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mboko alisema sekta ya afya itaimarika zaidi iwapo serikili kuu kupitia wizara ya afya nchini, itazitengea serikali za kaunti fedha za kutosha.
Kulingana na Mboko, sekta ya afya katika maeneo ya mashinani inapitia changamoto nyingi hata baada ya kugatuliwa kwa sekta hiyo, hali ambayo imechangiwa na ukosefu wa fedha katika hospitali za rufaa na zahanati, na kusababisha hudumu duni kwa wakazi.
“Serikali kuu lazima itutengee fedha za kutosha katika kaunti na kuimarisha hospitali zetu za rufaa na zahanati. Sisi kama viongozi tutahakikisha serikali kupitia wizara ya afya nchini imetenga fedha zaidi kwa serikali za kaunti,” alisema Mboko.
Aidha, alisema kwamba kuongezewa fedha zaidi katika sekta hiyo kutaufanikisha zaidi ugatuzi ikizingatiwa kwamba wizara hiyo ni moja wapo, kati ya sekta muhimu kwa wananchi.
Aliishinikiza serikali kuzingatia pendekezo hilo ili kuhakikisha huduma bora za kiafya zinatolewa kwa wakazi.
Kiongozi huyo alisema kwamba iwapo serikali itazidi kudidimiza juhudi za ugatuzi, basi atawashinikizi viongozi wengine bungeni kupitisha mswada wa kuondolewa mamlakani waziri wa afya nchini kwa kuonekana kushindwa kutekeleza majumu yake.
“Tuko tayari kuwashinikiza viongozi wengine bungeni kupitisha mswada wa kumuondoa mamlakani waziri wa afya kwa kushindwa kuimarisha sekta ya afya hasa katika kaunti na kuwasababishia wakazi changamoto nyingi za kiafya,” aliongezea Mboko.
Haya yamejiri huku bunge la kitaifa nchini likiandaa kuwasilisha mswada bungeni kupinga kugatuliwa kwa sekta ya afya na kuirejesha katika wizara ya afya nchini, chini ya serikali kuu.