Sheria ya kudhibiti utoaji wa leseni kwa wauzaji vileo katika Kaunti ya Mombasa inakumbwa na utata kufuatia kutoshirikiana kwa maafisa wa serikali ya kaunti na serikali kuu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa Idara ya Utalii na Utamadani katika Kaunti ya Mombasa Binti Omar, amesema kuna haja ya kila mmoja kuelewa majuku yake na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa kikamilifu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano wakati wa mkutano baina ya viongozi wa serikali na wafanyibiashara wa vileo na mikahawa, Omar alipinga madai kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa imejitenga na utendakazi wa serikali kuu.

Alisema kuwa maswala ya maendeleo na uwajibikaji yanafaa kutekelezwa vyema kwa wakaazi.

"Sisi tuko tayari kushirikiana na serikali kuu. Ni sharti serikali za kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana katika maswala ya kudhibiti uuzaji wa pombe,” alisema Omar.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mahmoud Salim alisema kuwa ukosefu wa mawasiliano ndio unaochangia pakubwa mizozo inayoendelea kwa sasa.

Alisema kuwa ufisadi ndio chanzo kikuu cha kushindwa kudhibiti uuzaji wa pombe haramu.