Waziri wa masuala ya afya kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Gladys Momanyi amesema kuwa wizara yake ina mipango ya kuanzisha ujenzi wa makao rasmi ya madaktari kwenye hospitali kuu ya kaunti ya Nyamira. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu katika shule ya upili ya Sironga kwenye hafla ya kongamano la pamoja lililohuzisha wizara zote za serikali pamoja na wananchi siku ya Alhamisi, Momanyi alisema kuwa wizara yake ina mikakati ya kuwajengea madaktari makazi yao kabla ya mwezi june mwakani. 

"Kwa sababu kama serikali tuna nia ya kuleta karibu huduma za afya kwa wananchi wizara yangu ina mipango ya kujenga makao rasmi ya madaktari kwenye hospitali kuu ya Nyamira ili kuwawezesha madaktari kukaa karibu na hospitali ili kuwahudumia wananchi kwa haraka," alisema Momanyi. 

Momanyi aidha alitangaza wazi kwamba serikali ya kaunti hiyo ina nia ya kujenga vyumba vitatu zaidi vya upasuaji kwenye hospitali kuu ya Nyamira ili kusaidia katika kukidhi mahitaji ya wagonjwa.

"Ili kukidhi mahitaji ya wananchi hasa wagonjwa walio na mahitaji ya kufanyiwa upasuaji serikali ya kaunti imetenga fedha zitakazotusaidia kujenga vyumba vitatu vya upasuaji," aliongezea Momanyi.