Serikali kupitia Wizara ya Elimu imesema itatoa mafunzo maalum kwa walimu wa shule za msingi na za upili kuhusu jinsi ya kuisimamia mitihani ya kitaifa ya darasa la nane KCPE na ya kidato cha nne KCSE.
Baraza la mitihani nchini KNEC linaitaka kila shule kuteua walimu wawili watakaotuma maombi ya kupokea mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza tarehe 14 mwezi Agosti hadi 27 mwaka huu.
Kulingana na KNEC mafunzo hayo yatasaidia kuboresha utahini na usahishaji wa mitihani hiyo na pia kupunguza hitilafu za mara kwa mara ambazo hukumba mchakato mzima wa mtihani nchini.
Walimu watakaotumia ombi la kushiriki mafunzo wanatakiwa kuwa na umri usiozidi miaka 50, wasiwe na rekodi ya utovu wa nidhamu kutoka kwa mwajiri wao TSC na pia lazima walimu wakuu wa shule husika watoe pendekezo rasmi.
Haya yanakuja wakati Waziri wa Elimu Fred Matiang’i mwezi uliopita alitangaza mabadiliko katika muhula wa tatu ikiwemo kuondoa hafla ya maombi ya kabla ya mtihani na kupiga marufuku wazazi kuwatembelea wana wao shuleni, hatua aliyotaja kama itakayosaidia kupunguza wizi wa mtihani.