Shughuli za uchukuzi katika Kaunti ya Mombasa zinatarajiwa kuimarika baada ya serikali kutangaza kuwa inanuia kufufua huduma katika kivuko cha Mtongwe.
Katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Irungu Nyakera amesema kuwa serikali imeweka mikakati ya kuimarisha sekta ya uchukuzi, hasa katika vivuko vya Likoni na Mtongwe.
Nyakera alisema kuwa hatua hiyo itachangia pakubwa katika kudhibiti msongamano vivukoni humo, pamoja na kuimarisha utalii katika ukanda wa Pwani.
“Serikali imetenga fedha za kutosha kuona kuwa kivuko cha Mtongwe kinarudi kutumika ili kupunguza msongamano wa watu na magari katika kivuko cha Likoni,” alisema Nyakera.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa feri ya MV Harambee, Nyakera alisema mipango imewekwa kuhakikisha wanafufua huduma katika Kivuko cha Mtongwe katika kipindi cha majuma mawili yajayo.
Vile vile, amedokeza kuwa takriban shilingi milioni 800 zimetengwa kukarabati feri zote za zamani ili kudhibiti visa vya feri hizo kukwama.
Itakumbukwa kwamba, usafiri katika Kivuko cha Mtongwe ulisitishwa kwa kipindi cha takriban miongo miwili iliyopita, kufuatia mkasa wa kuzama kwa feri ya MV Mtongwe iliyopelekea watu wasiopungua 260 kupoteza maisha yao.