Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amelalamikia kutengwa kwa eneo bunge lake na serikali ya Kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Hassan Joho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Likoni, Mwahima alisema kuwa toka kuingia uongozini, serikali ya Kaunti ya Mombasa haijatekeleza miradi yoyote ya maendeleo katika eneo bunge la Likoni, licha ya kuanzisha miradi katika maeneo bunge mengine.

Aidha, mbunge huyo alilalamikia hali mbaya ya barabara katika eneo hilo, pamoja na ukosefu wa maji safi, huku akisema kuwa wakaazi wanaendelea kuhangaika kutokana na hali duni ya maisha.

"Gavana Joho amekuwa akitembelea Kisauni, Mvita, Jomvu, Nyali na Changamwe akiendeleza maendeleo, jambo ambalo hatujaona Likoni," alisema Mwahima.

Itakumbukwa kuwa mbunge huyo alitangaza rasmi kuwa atashirikiana na serikali ya Jubilee katika kuleta maendeleo Likoni, jambo ambalo halijapokelewa vizuri na viongozi katika mrengo wa Cord.