Ni afueni kwa maskwota wanaoishi katika shamba lenye utata la Waitiki lililoko Likoni mjini Mombasa baada ya serikali ya kaunti hiyo kusema kuwa itagharamia ada ya umiliki ambayo serikali kuu iliwaagiza walipe.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika eneo la Mtongwe mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan aliitaja hatua ya serikali kuu ya kuwatoza ada maskwota hao kama ukandamizaji mkuu wa wasiojiweza katika jamii.

‘’Sijawahiona dunia hii maskwota wakiambiwa walipe ada ndio wapewe haki miliki, hii ya Mombasa inakera. Hiyo pesa wanataka wananchi walipe wakate kwa serikali ya kaunti,’’ alisema Joho.

Aidha Joho aliwataka maskwota hao kutolipa ada hiyo na kuahidi kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa itazungumza na serikali kuu ili kukubaliana namna pesa hiyo itakavyolipwa bila wakaazi hao kugharamika.

Mapema mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta aliwataka wakaazi wa shamba la Waitiki waliokabithiwa hati miliki kulipa ada ya umiliki ya shilingi elfu 82 katika kipindi cha miaka 12 ijayo.

Agizo hilo hata hivyo liliibua hisia kinzani kutoka kwa wakaazi na hata viongozi mbalimbali wa kisiasa kutoka ukanda wa Pwani ambao wengi wao walilipinga.