Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeanzisha mipango ya kutafuta sehemu itakayotumika kujenga soko katika wadi ya Kadzandani, eneo bunge la Nyali.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada wa wakaazi wa eneo hilo kusema kuwa kujengwa kwa soko katika eneo hilo kutasaidia pakubwa katika kuimarisha maswala ya biashara na kutoa nafasi za ajira kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao na wananchi kwenye uwanja wa Posta eneo la Kwa Bulo, Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho alisema kuwa mikakati ya kujenga soko katika eneo hilo imezingatiwa na tayari kinachosubiriwa ni kupatikana kwa sehemu mwafaka ya kufanya mradi huo.

“ombi lenu la soko limesikizwa na kuzingatiwa. Kinachotakiwa ni kupatikana kwa sehemu itakayotumika kuweka soko hilo,” alisema Joho.

Wanawake katika eneo hilo wametilia mkazo wazo hilo kwa kusema kuwa kubuniwa kwa soko hilo kutawaimarisha kibiashara na kuwatoa katika nyororo za kutegemea uuzaji wa pombe ya mnazi.