Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nakuru iko katika harakati za kutia saini mkataba wa ushirikiano na shirika la kilimo la Agricultural Development Corporation (ADC).

Hatua huyo inanuia kuimarisha na kuboresha kilimo katika kaunti hiyo.

Akizungumza alipomtembelea Naibu Gavana wa Kaunti ya Nakuru Joseph Ruto afisini mwake siku ya Alhamisi, afisa mkuu wa Shirika la ADC Dkt Andrew Tuimur alisema shirika hilo limeamua kushirikiana na kaunti ya Nakuru ili kuboresha kilimo cha viazi na kile cha mifugo miongoni mwa mambo mengine yanayohusiana na kilimo.

“Tunanuia kuongeza kiwango cha mbegu za viazi kwenye kaunti ya Nakuru, jambo ambalo tumelipa kupaumbele. Tutahakikisha hakuna upungufu wa mbegu hizo kwenye kaunti na katika taifa la Kenya kwa jumla,” alisema Dkt Tuimur.

Musa Sirma, mwenyekiti wa ADC alisema ushirikiano kati ya shirika hilo na kaunti ya Nakuru unalenga kuboresha kilimo na kuongezea kwamba ushirikiano huo utabadili maisha ya wakazi wa Nakuru.

“Ugatuzi ulianza kutekelezwa kwa kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa mbali na watu wake. Serikali za kaunti zinafaa kuwa karibu na Wakenya na kuleta rasilimali karibu nao,” alisema Sirma.

Naibu Gavana Joseph Ruto aliyekuwa ameandamana na Afisa mkuu wa kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenye kaunti ya Nakuru Purity Muritu na mwenzake wa Idara ya Barabara mhandisi Samwel Mwaura pamoja na mkuu wa Idara ya ardhi kwenye kaunti ya Nakuru Rachael Maina miongoni mwa maafisa wengine wa kaunti ya Nakuru, alikaribisha ushirikiano huo.