Katika juhudi za kukabiliana na mkurupuko wa maradhi, hasa ongezeko la visa vya homanyongo yaani Hepatitis A katika Kaunti ya Mombasa, sasa serikali ya kaunti hiyo imezindua mpango wa kuyatibu maji katika kaunti hiyo.
Akitangaza hatua hiyo baada ya kuzuru maeneo mbali mbali kisiwani Mombasa kukagua hali ilivyo katika visima vya mji huo, Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa Francis Thoya alisema kuwa maji yanayotumiwa na wakazi yanastahili kutibiwa ili kuzuia maradhi.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Thoya alieleza kuwa Kisiwani Mombasa pekee kuna zaidi ya visima elfu moja ambavyo havijatibiwa kwa muda mrefu, na kufikia sasa zaidi ya visima 100 tayari yametibiwa, huku wale wanaomiliki visima wakipewa dawa za chlorine kutibu maji yao.
“Tuko na visima elfu moja na bado havijatibiwa hali hiyo inatia hofu wakaazi ya kuzuka kwa maradhi hasa msimu huu wa mvua lakini umetia juhudi kubwa na kumetibu tayari visima 100 kwa hivyo tuko na nia kama serikali ya kaunti ya Mombasa kuzuia kuchupuka kwa maradhi,” alisema Thoya.
Kwa upande wao wakazi wamekiri kukabiliwa na changamoto ya kupata vidonge vya kutibu maji, kwa kuwa hapo awali walikuwa wakipata dawa hizo kila baada ya miezi mitatu.
Juhudi za serikali ya kaunti hiyo zinajiri baada ya kaunti hiyo kuripoti mkurupuko wa homanyongo, ambapo katika kipindi cha juma moja tu, jumla ya visa 114 vimeripotiwa katika Hospitali Kuu ya Ukanda wa Pwani.