Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama na wawekezaji wa kampuni ya ujenzi wa makazi almaarufu Mock Gardens wameandikisha mkataba wa ujenzi wa jiji jipya katika kaunti ya Nyamira kwa kima cha shillingi billioni 12.
Akiwahutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumatano baada ya kufanya kikao na mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Aaron Nyamboki, gavana Nyagarama alisema serikali yake imeweka mikakati ya kujenga jiji katika kaunti hiyo.
"Tunajaribu kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunajenga jiji jipya katika kaunti hii ila changamoto ambayo tunayo ni kutokuwepo kwa ardhi ya serikali ili kujenga jiji hilo," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kwa kusema kuwa serikali yake imeanzisha mikakati ya kuwarahi wakazi wa kaunti hiyo kupeana ardhi zao ili kuruhusu ujenzi wa jiji hilo kuanzishwa.
"Kwa vile hamna ardhi ya kutosha huku Nyamira, kama serikali tumeanza kuwarahi wakazi wa kaunti hii ambao wana ardhi ambazo wameshindwa kuzistawisha kuepeana ardhi hizo kwa serikali ili kuruhusu ujenzi huo kufanyika," aliongezea Nyagarama.