Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya kaunti ya Nakuru imesema kuwa itawaajiri wauguzi zaidi katika hospitali zake, ili kukabiliana na upungufu wa wahudumu hao wa afya katika kaunti hiyo.

Utawala wa kaunti hiyo aidha ulisema hautawekeza katika ujenzi wa vituo vingine vipya vya afya, ila utaelekeza nguvu zake katika kuwaajiri wahudumu kwenye vituo vya afya vilivyoko kwa sasa.

Akizungumza mjini Naivasha Jumatatu, naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto alisema hayo.

“Nakuru ina vituo vingi vya afya ambavyo havina wauguzi wa kutosha. Hilo ndilo jambo ambalo tutapea kipau mbele, kuwaajiri wahudumu ambao watafanya kazi katika hospitali hizo ikiwemo zile ambazo zimejengwa na serikali ya kaunti katika wadi mbali mbali,” Ruto alisema.

Ripoti iliyotolewa majuma kadhaa yaliyopita na chama cha wauguzi nchini KMMPDU, ilisema kuwa Kenya inahitaji wauguzi elfu 83 zaidi, ili kuafikia idadi inayokubaliwa na shirika la afya duniani WHO.