Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Bunge la Kaunti ya Mombasa Kibwana Baya amependekeza kuboreshwa kwa zahanati ziliko katika kaunti hiyo ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali kuu ya Pwani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Baya, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Miritini, alisema kuwa hali ya idadi kubwa ya wagonjwa kusongamana katika hospitali hiyo inayohudumia wakaazi wote wa ukanda wa Pwani, imechangia kuwepo kwa huduma duni kwa wakaazi.
Baya alipendekeza dawa na vifaa muhimu vya matibabu kuekezwa zaidi katika zahanati za Kaunti ya Mombasa, kama njia moja ya kuimarisha huduma kwa wakaazi na kupunguza msongamano katika hospitali hiyo kuu ya Pwani.
Aidha, alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa inafaa kutenga fedha zaidi za kuimarisha maendeleo ya kaunti hasa katika makadiro ya bajeti pamoja na kuzingatia ukusanyaji ushuru wa kaunti.
"Serikali ya Kaunti ya Mombasa inafaa kuchukulia swala hii kwa uzito na kuboresha zahanati zetu kwa kuweka dawa na vifaa vingine muhimu vya matibabu ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa katika Hospitali kuu ya Pwani,” alisema Swaleh.
Kiongozi huyo aliahidi kulishinikiza Bunge la Kaunti ya Mombasa kufanikisha ahadi walizoweka kwa wakaazi wakati wa kampeni za kisiasa mwaka wa 2013.