Serikali ya Kaunti ya Nyamira imehimizwa kuanzisha mbinu mpya za kukarabati barabara ili kuwaepusha wakazi kutokana na changamoto za hali mbovu ya barabara.
Akihutubia wakazi wa Gesima siku ya Jumatatu, Shadrack Okioge, ambaye ni mhandisi, alishtumu serikali ya kaunti kwa kusema kuwa haikuwa na mipango mwafaka ya jinsi ya kukarabati barabara hizo, ila tu ilianza kuzikarabati baaada ya wakazi wa maeneo husika kulalamika.
"Mimi ni mhandisi ninaye shughulikia kazi za ujenzi na miundomisingi na ukweli ni kuwa serikali ya kaunti hii haijaweka mikakati yakutosha kuhakikisha kuwa barabara zinakarabatiwa kwa njia inayofaa," alisema Okioge.
Okioge alisema kuwa huenda serikali ya kaunti hiyo ikapoteza pesa za umma kupitia kwa wanakandarasi ambao hawajaweka mipango mahususi ya kukarabati barabara za eneo hilo.
"Kwa vile serikali ya kaunti haijakuwa na mipango maalum yakukarabati barabara, huenda ikapoteza pesa nyingi kupitia kwa wanakandarasi walio na nia yakuibia serikali,” alisema Okioge.
Okioge aidha alisema kuwa iwapo mipango maalum itawekwa, serikali ya kaunti hiyo itafanikiwa pakubwa kukabiliana na wizi wa pesa za umma kwa kuwa barabara zinafaa kukarabatiwa moja baada ya nyingine.
"Lazima serikali ya kaunti iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa barabara zinakarabatiwa moja baada ya nyingine ili kuwe na uwazi na uwajibikaji miongoni mwa wanakandarasi," alisema Okioge.