Serikali ya Kaunti ya Mombasa imehimizwa kuwatambua kikamilifu watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo na kubadili hali yao ya maisha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mwakilishi mteule katika bunge la Kaunti ya Mombasa Hurdson Karume, alisema kuwa jamii ya walemavu katika kaunti hiyo imekumbwa na changamoto nyingi mno za maisha.

Alisema kuwa changamoto hizo zinapaswa kutatuliwa ili kutoa mazingira bora kwa jamii hiyo ya walemavu.

Karume alisema kwamba ni muhimu kwa watu wanaoishi na ulemavu kuhusishwa na kutengewa miradi mbalimbali itakayowawezesha kujikimu kimaisha.

Alisema kuwa amesikitishwa na hali duni ya maisha na vikwazo vingi vya kiuchumi wanavyopitia walemavu, huku akiishinikiza serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwaangazia zaidi walemavu katika Kaunti hiyo.

"Tunaiomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kututambua sisi kama jamii ya walemavu ili kuhakikisha kuwa maswala muhimu ya maendeleo inatekelezewa,” alisema Karume.

Karume alisema kwamba kama mwakilishi wa walemavu katika bunge hilo la Kaunti ya Mombasa, atashinikiza mgao zaidi kwa jamii ya walevu ili waidhinishe miradi itakayoimarisha hali yao ya maisha.

Hatua ya Karume inajiri siku chache tu baada ya jamii ya walemavu katika eneo la Bamburi kulalamikia kubaguliwa na serikali na kaunti kwa kushindwa kuwajengea miundo msingi ikiwemo shule maalum za watoto walemavu.