Wakenya wanaposherehekea msimu wa Krismasi kwa njia mbalimbali, serikali ya Kaunti ya Nyamira inaendelea kukadiria hasara baada ya afisi zake kule Keroka kuteketea na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali usiku wa mkesha wa Krismasi.
Akithibitisha kisa hicho OCPD wa Borabu Peter Nyongesa alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana ila maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.
"Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hiki kwa maana chanzo cha moto huu hakijajulikana," alisema Bw Nyongesa.
Kwa upande wake, Katibu wa uajiri kwenye kaunti hiyo Erick Aori alihoji kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati kuhakikisha utoaji huduma kwa wakazi wa Keroka na vitongoji vyake hazitathiriki kutokana na kisa hicho.
"Kama serikali tumeweka mikakati kuhakikisha kuwa shughuli za utoaji huduma kwa wakazi wa Keroka haziathiriki kivyovyote huku tunapo tafuta mbinu zakujenga afisi hizi upya," alihoji Aori.
Kwa muda sasa wanabiashara wa eneo hilo wamekuwa wakidinda kulipa ushuru kwa serikali ya kaunti hiyo kwa kile wanacholalamikia kuwa huduma duni wanazopokezwa na serikali.