Mwakilishi wa Wadi ya Miritini, Kaunti ya Mombasa, Kibwana Swaleh, ameilaumu serikali ya kaunti kwa kufeli katika kukabili majanga kila yanapotokea.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kibwana alidai kuwa kila kunapotokea mkasa wa dharura, maafisa wanaohusika na shughuli ya kuwaokoa wakaazi huchukua muda mrefu kabla kufika katika eneo la tukio.

Akizungumza katika eneo la Mkupe huko Miritini siku ya Jumatatu, baada ya mwanafunzi mmoja wa shule ya upili kuzama alipokuwa akiogelea na wenzake, kiongozi huyo alishangazwa na hatua ya wanajeshi wa majini wa Kenya Navy kuchelewa kufika eneo hilo, na kusema kuwa serikali ya kaunti inafaa kuweka vitengo maalum vya kukabiliana na dharura badala ya kutegemea serikali kuu peke yake.

Inadaiwa kijana huyo, Ayub Salim, alilemewa na mawimbi mazito kabla kuzama, huku wanakijiji wakiwalaumu maafisa wa Kenya Navy kwa kuchelewa kufika licha ya kufahamishwa mapema.

“Sio mkasa huu peke yake. Hata kunapotokea ajali ya moto, hali huwa hivi ambapo wananchi huumia kabla ya kupata msaada,” alisema Kibwana.

Aidha, kiongozi huyo alisema atawasilisha mswada katika kamati ya kushughulikia dharura bungeni, ili kutafuta suluhu ya jinsi ya kukabili mikasa kama hiyo.

“Katika bunge letu la kaunti tuko na kamati ya mambo ya dharura. Nitapeleka hoja hiyo bungeni kwa sababu haya ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipao mbele,” alisema Kibwana.

Maafisa wa jeshi la wanamaji la Kenya Navy walifanikiwa kupata mwili wa kijana huyo siku ya Jumanne kabla ya kufanyiwa mazishi baadae.