Zaidi ya wanachama mia nane wa muungano wa wauzaji maji katika eneo bunge la Kisauni, wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuboresha huduma za kusambaza maji kwa wananchi katika eneo hilo.
Aidha, wanachama hao waliitaka serikali ya kaunti kukoma kusitisha huduma hizo kila wakati bila kuwafahamisha lolote.
Akizungumza siku ya Alhamisi jijini Mombasa baada ya kuandaa mkutano na wanachama, mwenyekiti wa muungano huo Ben Ndege, alisema kuwa hatua ya kukatiwa maji si sawa kwani wanalipa bili za maji na kulipa leseni mapema bila kuchelewa.
“Serikali ya Kaunti ya Mombasa inataka kukandamiza wananchi kwa kukata maji ikidai kuwa ni njia mojawapo ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa homanyongo ambao umezuka hivi karibuni. Hatutakubali haya yatendeke na iwapo kuna sababu yoyote yenye kuaminika, basi ni lazima watueleze waziwazi,” alisema Bw Ndege.
Aidha, Bw Ndege aliitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kutibu maji ya mabomba ili kuhakikisha kuwa wakaazi wanapata maji safi.
Aidha, alisema kuwa wauzaji wa maji ya kisima na wahudumu wa mikokoteni wanapaswa kupewa sheria mwafaka ili kuzuia kuenea kwa magonjwa mbali mbali yanayoenezwa na maji machafu.