Wakazi wa kaunti ndogo ya Masaba Kaskazini, wameiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kuhakikisha kwamba ambulensi zinapatikana vijijini ili kusaidia kwenye utoaji wa huduma za dharura.
Akiongoza wakazi hao, diwani wa zamani wa Gachuba, Bw Willis Kanyimbo, aliyekuwa akizungumza siku ya Jumapili alisema kuwa ambulensi hizo zilizonunuliwa na serikali ya kaunti hazitakuwa na umuhimu wowote ule iwapo hazitawahudumia wananchi vijijini.
"Magari ya ambulensi hayatakuwa na umuhimu wowote ule iwapo hayatopatikana vijijini kuwahudumia wananchi wanao hitaji huduma hizo za dharura,” alisema Kanyimbo.
Kanyimbo alisema kuwa huduma za dharura ni haki ya kila mwananchi kwa kuwa wao ndio hulipa ushuru huku akiongeza kuwa iwapo magari hayo yatafika vijijini, yatawasaidia wananchi wengi.
"Utoaji wa huduma za dharura ni haki ya kila mwananchi kwa kuwa wananchi ni walipa ushuru na iwapo basi gari hizo zitafika vijijini wakazi wengi watasaidika pakubwa,” aliongezea Kanyimbo.
Kanyimbo aidha alilalamikia huduma za polepole zinazo tolewa na ambulensi hizo hali inayo sababisha wananchi wengi kupoteza maisha yao.
"Ninalalamikia huduma za polepole zinazo tolewa na ambulensi hizo hali inayosababisha wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura kupoteza maisha yao. Ninaomba maafisa husika kuimarisha huduma hizo,” aliongezea Kanyimbo.
Hata hivyo, katibu wa wizara ya afya kwenye kaunti ya Nyamira Douglas Bosire alipuuzilia mbali madai kuwa huduma za ambulensi huwa ni za polepole.
"Madai kuwa huduma za magari ya ambulensi katika kaunti hii ni za polepole sio ya kweli na ninawaomba wananchi wanaohitaji huduma hizo kuwasiliana na afisi za kaunti ndogo ili kupata usaidizi,” alisema Bosire.