Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi kutoka wadi ya Rigoma eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira wameiomba serikali ya kaunti hiyo kujenga zahanati katika kila wadi ili kuimarisha sekta ya afya katika kaunti nzima ya Nyamira.

Hii ni baada ya serikali ya kaunti ya Nyamira kutenga shillingi billioni 1.5 katika sekta ya afya.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika uwanja wa shule ya msingi ya Rigoma iliyoko wadi ya Rigoma, wakazi hao walisema zahanati zinastahili kujengwa kwa kila wadi zote ishirini zilioko kwa kaunti hiyo ili kuimarisha sekta ya afya kikamilifu.

“Tunaomba serikali yetu ya kaunti kuongeza zahanati katika wadi zote za kaunti hii maana pesa zilizotengewa sekta ya afya ni nyingi mno,” alisema Wilfred Mokua, mkazi wa wadi ya Rigoma.

Aidha, wakaazi hao waliomba serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa imefadhili zahanati hizo dawa za kutosha ili wakazi wasiwe wakiteseka na kulazimika kunua dawa kutoka hospitali za kibinafsi.

“Pindi zahanati hizo zitakapojengwa lazima zinunuliwe dawa za kutosha. Hakuna haja ya kutumwa kwa zahanati ya kibnafsi kununua dawa. Serikali ina pesa nyingi za kushughulikia mambo hayo yote,” alisema Winfridah Osoro, mkazi.