Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kumlipa fundi aliyetengeneza lango la kichinjio cha daraja alilolitengeneza mapema mwaka huu.
Wito huo umetolewa baada ya fundi huyo kwa jina Robert Mayworo kutolipwa kwa kazi aliyoifanya kwa mwiezi kadhaa iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, fundi Robert Mayworo alisema serikali ya kaunti hiyo ilimkabidhi kibarua cha kutengeneza lango hilo kwa shillingi 58,000 na baada ya kumaliza kutengeneza lango hilo hajawahi lipwa hata shillingi moja ilhali lango hilo lilitolewa kwake na kuahidiwa kuwekewa pesa kwa akaunti yake.
Kulingana na fundi huyo, lango hilo lilitolewa kwake akiahidiwa kuwekewa pesa zake kwa akaunti jambo ambalo halijawai kushughuliwa na kumsababishia hasara kwani alinunua vyuma na pesa kutoka kwa mfuko wake.
“Tangu nimalize kutengeneza lango ambalo ni la kichinjio cha daraja mbili sijawahi lipwa pesa hizo ambazo tulielewana na maafisa wa serikali hii ya Kisii shillingi 58,000,” alisema Mayworo.
"Naomba nilipwe pesa hizo ili niendeleze biashara zangu kwani biashara yangu imerudi nyuma maana nilitumia pesa za biashara kulitengeneza lango hilo la kichijio cha daraja mbili,” aliongeza.
Robert anasema kuwa walipofuatilia pesa hizo, mwenyekiti anayesimamia utumizi wa pesa za serikali katika kaunti ya Kisii Ronald Onduso alishangazwa na mambo hayo na kumwahidi kufuatilia ili alipwe pesa zake.