Serikali ya kaunti ya Nyamira imepongezwa kwa kuwaajiri wahudumu wa afya katika hospitali.
Hii ni baada ya kaunti hiyo kuwa na upunguvu wa wahudumu wa hospitali, jambo ambalo lilipelekea wakazi kuiomba serikali hiyo kuchukua hatua ili kuboresha huduma za afya.
Sasa, serikali ya kaunti imewaajiri wahudumu mia mbili ishirini na sita ambao wameanza kazi rasmi katika hospitali zote za kaunti hiyo, jambo ambalo limewafurahisha wakazi na maafisa wa serikali.
Akizungumza siku ya alhamisi katika shule ya upili ya Kebirigo, waziri wa afya Douglas Bosire aliipongeza serikali hiyo kwa kuwaajiri wahudumu wa afya katika hospitali, huku akisema hiyo ni maendeleo.
Hata hivyo, Bosire alisema gavana John Nyagarama ameimarisha sekta ya afya zaidi, huku akimwomba kuendelea kuongeza wahudumu wa afya ili kuboresha huduma za matibabu kwa serikali za kaunti hiyo.
“Naipongeza serikali ya kaunti yetu ya Nyamira kwa kuongeza wahudumu mia mbili na ishirini na sita hivi maajuzi na tayari wameanza kutoa huduma za matibabu katika hospitali zetu. Naomba gavana kuendelea na motisha hiyo ya kuajiri wengi,” alisema waziri.
Bosire aliomba wahudumu hao kufanya kazi jinsi inavyohitajika kwani wamepokezwa kazi ya kushugulikia huduma ya matibabu.