Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa imeshinikizwa kuyaangazia maeneo yanayokumbwa na tatizo la funza katika kaunti hiyo, ili kuthibiti tatizo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na shirika la vijana linaloangazia masilahi ya vijana na wakongwe katika eneo la Kisauni la ‘Suluhisho Youth and Elderly Empowerment,’ tatizo la funza limeathiri maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo, huku baadhi ya watoto wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na athari za wadudu hao.

Akizungumza kwenye mkutano wa hamasa katika eneo la Kiembeni huko Kisauni siku ya Alhamisi, mkurugenzi wa shirika hilo George Riri, alisema kwamba maeneo ya Nguuni, Kiembeni, Bombo na Mireroni, ni baadhi ya maeneo yaliyoathirika na funza.

Riri alisema kwamba japo kundi hilo la vijana limekuwa lishughulikia tatizo hilo la kiafya tangu mwaka jana, ukosefu wa fedha, wataalamu wa afya na dawa za kuwatibu waathiriwa hao umekuwa kikwazo kikuu katika shirika hilo.

Aidha, ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuliwajibikia tatizo hilo la kiafya katika kaunti hiyo na kukabiliana vyema na mdudu huyo anayeathiri maisha ya jamii.

“Tunaitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuingilia kati na kusaidia jamii kukabiliana na funza ili kuokoa maisha ya wakaazi,” alisema Riri.

Riri aliikosoa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa kwa kushindwa kuchukua hatua zozote ili kukabiliana na tatizo hilo licha ya kuarifiwa kuhusiana na hali hiyo katika maeneo bunge ya Kisauni na Jomvu.