Serikali ya Kaunti ya Mombasa imewahimiza wakaazi wanaoishi katika maeneo ya mabonde kuhamia maeneo ya juu msimu huu wa mvua ili kuepukana na hatari ya maporomoko.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa Kaunti ya Mombasa Francis Thoya amesema kuwa tayari wameweka mikakati ya kuzuru mashinani ili kuwahamasisha wakaazi kuhusu athari za mvua kubwa.

Kwenye kikao na wanahabari afisini kwake mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Thoya alisema kuwa maeneo yanayokisiwa kushuhudia maporomoko na mafuriko ni yale ya Kalahari, Bokole, Tudor Moroto, Mburukenge, Junda na Jomvu.

"Tunawaagiza wakaazi wanaoishi maeneo ya mabonde kuhamia maeneo ya juu ili kuzuia kushuhudiwa kwa maporomoko na mafuriko, hasa wakati huu ambapo mvua inaendelea kunyesha Mombasa,” alisema Thoya.

Aidha, katibu huyo alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo inalenga kutenga shilingi milioni 20 kushughulikia ukarabati na ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji taka pamoja na kutibu maji ya visima na mifereji ili kuzuia kushuhudiwa kwa mkurupuko wa maradhi.

Alisema kuwa serikali ya kaunti itajitahidi kuzuia athari zinazotokana na mvua kubwa ili kuhakikisha kuwa wakaazi wa Mombasa wanaishi katika mazingira yaliyoboreshwa.