Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wavuvi kaunti ya Mombasa wana matumaini baada ya serikali ya kaunti hiyo kuandaa kongamano na wanachama kutoka sekta ya uvuvi kujadili mikakati ya kufufua biashara hiyo inayoonekana kudidimia.

Akiongea wakati wa kongamano hilo siku ya Jumanne mjini humo, waziri wa biashara na uvuvi kaunti hiyo Anthony Njaramba alisema kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wavuvi wananufaika na biashara hiyo.

Serikali hiyo ya kaunti inasema imepata mkopo wa Sh30 milioni za kutengeneza boti mbili mpya za uvuvi ambapo shughuli hiyo tayari imeanza.

Kwa upande wake mkurugenzi katika sekta ya uvuvi kaunti hiyo Collins Ndoro amesema boti hizo zitasaidia wavuvi kufanya uvuvi hadi kwenye maji mengi.

“Tunataka wavuvi wetu watoke kwenye uvuvi wa maji machache waingie mpaka ndani kwenye maji mengi, tuna matuaini kufikia mwezi wa pili hapo mwakani hizo boti zitakuwa tayari na wavuvi watakuwa wanaweza kukaa kwenye maji hadi wiki mbili wakifanya uvuvi bila wasiwasi,” alisema Ndoro.

Kongamano hili linajiri siku chache baada ya mwandishi wetu kutembelea soko kuu la samaki la Old Town na kukutana na wavuvi walioeleza masikitiko yao kutotambuliwa na serikali.