Serikali ya kaunti ya Mombasa imezindua rasmi ruwaza yake ya mwaka 2035. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ruwaza hiyo inajumuisha mpangalio mpya wa kisasa wa jiji la Mombasa utakaobadilisha taswira ya jiji hili katika sekta mbali mbali. 

Akihutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi huo iliyoandaliwa kwenye uwanja wa Mombasa Golf, gavana wa Mombasa Hassan Joho ameeleza kuwa mpangilio huo utaifanya kaunti ya Mombasa kuwa ya kwanza kuanzisha mfumo wa kutibu maji ya bahari kutumika nyumbani hali itakayomaliza tatizo la uhaba wa maji linaloonekana kuwa donda sugu. 

Aidha ameongeza kuwa uchumi wa jiji unatarajiwa kukuwa kwa kiasi kikubwa kwa kukamilika kwa ruwaza hiyo pamoja na huduma bora za matibabu kwa wakaazi wa Mombasa. 

Kulingana na mpangilio huo, ujenzi upya wa nyumba zinazomilikiwa na serikali ya kaunti, ndio mradi wa kwanza kutekelezwa chini ya ruwaza hiyo, ambapo wananchi watapata fursa ya kumiliki nyumba hizo za kisasa. 

Licha ya kuzinduliwa kwa ruwaza hiyo, wakaazi wa Mombasa wamekuwa na hisia tofauti kuhusiana na mpango huo wa gavana Joho na serikali yake. 

Julius Ogogo mkeretwa wa masuala ya maendeleo hapa Mombasa ameutaja uzinduzi wa ruwanza hiyo kama uhusiano mwema na kujipigia debe kwa gavana Joho hasa baada ya kutangaza hadharani azma yake ya kutaka kuwania urais mwaka 2022.