Kufuatia hatua ya serikali ya taifa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa wa surua, serikali ya Kaunti ya Nyamira imeweka mikakati ya kuanzisha kampeni hiyo mapema juma lijalo.
Akiwahutubia wanahabari kwenye mkutano wa washikadau mjini Nyamira siku ya Alhamisi, waziri wa afya kwenye kaunti hiyo Gladys Momanyi alisema serikali ya kaunti hiyo inanuia kuwapa chanjo watoto elfu 276 walio na umri wa kati ya miezi tisa hadi miaka 14.
"Tunanuia kuwapa watoto elfu 276 chanjo dhidi ya ugonjwa wa ukambi na Rubella kuanzia tarehe 16 mwezi huu, na hii ni kampeni inayonuia kuwafaidi watoto walio na kati ya umri wa miezi tisa hadi miaka 24," alisema Momanyi.
Momanyi aidha aliongeza kwa kusema kuwa njia ya kipekee ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo ni kuwapa chanjo watoto kwa wakati unaofaa.
"Himizo langu kwa wazazi na walezi ni kuhakikisha kuwa watoto wanapewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa ukambi kwa kuwa hiyo ndio tu njia ya kipekee ya kuhakikisha watoto wamepata kinga," aliongezea Momanyi.