Wiziri ya Utalii nchini Najib Balala ameahidi kuimarisha utalii wa eneo la Pwani hususana katika kaunti ya Lamu, licha ya eneo hilo kukumbwa na changamoto za kiusalama na kupelekea kuzoroteka kwa sekta hiyo na uchumi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano baada ya kongamano la wadau wa sekta ya utalii, Balala amesema kuwa serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa marufuku iliyowekwa na mataifa ya magaharibi kuhusu raia wao kutozuru kaunti ya Lamu inaondolewa.

Balala anasema kuwa furaha yake ni kuona utalii wa Lamu ukiimarika hata zaidi kama ilivyokuwa miaka ya awali pamoja na kuimarishwa kwa usalama wa kaunti hiyo ili kuwavutia wageni zaidi.

Waziri huyo wa utalii ameahidi kushirikiana na serikali ya kaunti ya Lamu katika kuimarisha sekta ya utalii na usalama ili kuona kuwa uchumi wa kaunti hiyo na Kenya kwa jumla unaimarika hata zaidi.

"Tunafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa utalii wa eneo la pwani na hususan katika kaunti ya Lamu inaimarika na kukuza uchumi wa taifa hili, na kuhakikisha kuwa marufuku ya raia wa mataifa ya magharibi kutozuru Kenya inazidi kuondolewa," alisema Balala.

Marufuku ya raia wa kigeni kutozuru kaunti ya Lamu imejiri baada ya kaunti hiyo kukumbwa na msukosuko wa kiuslama tangu mwaka wa 2014.

Waziri wa Utalii nchini Najib Balala akizungumza na wanahabari kuhusu uimarishaji wa utalii eneo la pwani na hususan kaunti ya Lamu.