Serikali imehimizwa kuyachunguza mashirika na watu wanaosimamia ugavi wa chakula kwa waathiriwa wa baa la njaa ili kuzuia wizi wa vyakula hivyo.
Katibu mtendaji wa Baraza la maimamu na wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohamed Khalifa, amesema kuwa kuna madai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiiba chakula hicho na kukosa kuwasaidia waathiriwa.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Sheikh Khalifa alisema kuwa kitendo hicho kina wakandamiza na kuwanyima haki waathiriwa wa baa la njaa.
“Ni jambo la kusikitisha kusikia kuwa kuna baadhi ya watu wanakandamiza haki za waathiriwa na kuwanyima nafasi ya kupata msaada. Serikali inapaswa kuchunguza hatua hiyo na kuwachukulia hatua wanaohusika katika njama hiyo,” alisema Sheikh Khalifa.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza kuu la waislamu nchini SUPKEM ukanda wa Pwani Sheikh Muhdhar Khitamy, ameitaka serikali kuu kufuatilia utumizi wa fedha katika serikali za kaunti hasa katika eneo la Pwani.
Khitamy alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa serikali hizo zimeshindwa kutenga fedha za kukabiliana na baa la njaa.