Serikali imehimziwa kulishughulikia swala la kuwalipa fidia wakaazi wa eneo la Dongo Kundu ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara hiyo inatarajiwa kujengwa kutoka Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa kuelekea kusini mwa Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Watalii nchini, Mohammed Hersi, amesema kuwa iwapo swala hilo litatatuliwa kwa wakati mwafaka, basi maswala ya uimarishaji wa sekta ya utalii nchini yatapigwa jeki.
Kwenye mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Jumatano, Hersi alisema kuwa wageni wanaozuru humu nchini kupitia Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi hukumbwa na changamoto za kiusafiri kutokana na kushuhudiwa kwa misongamano katika kivuko cha feri cha Likoni.
"Tunaiomba serikali kuharakisha mpango wa kuwalipa fidia wakaazi wa Dongo Kundu na kupeana nafasi ya ujenzi wa barabara itakayosaidia kuimarisha shughuli za utalii nchini,” alisema Hersi.
Hersi alisema kuwa iwapo barabara hiyo itajengwa haraka, basi swala la uchukuzi wa watalii kutoka kiswani Mombasa hadi Pwani kusini litakuwa kwa urahisi kwani wengi wa watalii hao watatumia barabara hiyo ya Dongo Kundu.
Wadau hao wa sekta ya utalii nchini na hususan eneo la Pwani wameahidi kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Utalii nchini ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inaimarishwa.